SERIKALI YATENGA Sh. Mil. 500 KUUKABILI UGONJWA WA DENGUE

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetenga shilingi milioni 500 kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya "Dengue" ambao umesababisha vifo vya watu watatu kuanzia Januari mpaka mwezi huu.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Kebwe Stephen Kebwe amesema tangu ugonjwa huo ugundulike nchini, wagonjwa waliothibishwa kuugua ugonjwa huo ni 450 na kati ya hao wagonjwa wapya 60 wamegundulika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.Pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kupambana na ugonjwa huo kama kutoa elimu kwa wananchi, Timu ya Taifa ya maafa kukutana mara mbili kwa wiki ili kutathimini mikakati ya dharura, Naibu waziri huyo amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kwani maambukizwi ya ugonjwa huo hayatokani na kumhudumia mgonjwa au kumgusa.Katika hatua nyingine Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dokta Hussein Mwinyi amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2014/2015.Amewahakikishia watanzania hali ya usalama nchini kuwa ni shwari licha ya kuwepo kwa matishio na mashambulizi ya kigaidi katika eneo la Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Msemaji kutoka kambi ya Upinzani kwa wizara hiyo Masoud Abdallah Salim yeye ameitaka Serikali kuwakumbuka na kuwathamini wanajeshi wastaafu.Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ili iweze kutekeleza majukumu yake imeidhinishiwa shilingi trilioni 1.2 ilizozitenga katika bajeti ya mwaka 2014/2015.
Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 249 zitatumika katika miradi ya maendeleo.