Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (kushoto), Mwenyekiti Mtendaji wa
Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said
Meck Sadik (kulia), wakiwa kwenye sherehe za Maulid kukumbuka kuzaliwa
kwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja,
Dar es Salaam juzi usiku.
Kwa ufupi
“Ninaomba Waislamu na watu wa dini nyingine kuwa
pamoja, tuondoe tofauti zetu kwani sisi Watanzania ni watu tuliozoeleka
kwa kuwa na amani, nisingependa kuona dini zetu zinasababisha uvunjifu
wa amani.”
Dar es Salaam/Mikoani. Viongozi mbalimbali wa
siasa na Kiislamu nchini, wamehimiza amani, umoja, mshikamano wa
Watanzania ili kuliepusha taifa na balaa la kupoteza amani.
Walisema hayo katika maadhimisho ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyofanyika juzi usiku.
Rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliwataka
watu wa dini zote kuondoa tofauti zao ili kudumisha amani iliyopo nchini
kwa muda mrefu na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bin Simba
amewataka Waislamu nchini kuepuka migogoro ndani ya misikiti inayoweza
kuwagawa.
Mufti
Akihutubia mhadhara wa kitaifa wa Waislamu
uliofanyika kwenye Viwanja vya Stendi ya Ujiji, Kigoma, Mufti Simba
aliwataka waumini wa dini hiyo kuepuka migogoro ndani ya misikiti
inayoweza kuwagawa na kuzusha vurugu miongoni mwao.
Alisema migogoro na vurugu ndani ya misikiti
imesababisha Waislamu kukosa nguvu na umoja miongoni mwao na kujikuta
wakipoteza fursa ya kupiga hatua za maendeleo kwa kujenga miundombinu ya
kijamii kama vile shule, vyuo vikuu na hospitali.
“Ninawaasa Waislamu kuwa makini na baadhi ya watu
wanaotaka kutugawa kwa masilahi yao binafsi. Tuepuke sana migogoro baina
yetu ndani ya misikiti, wale wanaouza viwanja vya misikiti na mali za
Waislamu hawana budi kuacha mambo hayo mara moja kwa vile ndiyo kiini
cha migogoro mingi.
“Tujifunze kwa wenzetu Wakristo ambao kila
wanapopata viwanja, huvitumia kujenga miundombinu ya shule, vyuo na
hospitali ambazo mwishowe zinatusaidia hata sisi Waislamu kupata
maarifa. Hapa ndipo tunapotakiwa tujifunze kufanya mema ndani ya jamii
zetu kwa faida ya taifa na Waislamu wenzetu.”
Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid
Jongo aliwataka Waislamu kuacha kulalamika kwamba Serikali
inawakandamiza Waislamu na kuwapendelea Wakristo akisema jambo hilo si
kweli.
“Waislamu tumekuwa tukilalamika kwamba kuna
mfumo-kristo unaofanya kazi ndani ya Serikali na utawala wa nchi yetu.
Hizi tuhuma si za kweli na hazipo kabisa. Zaidi kinachotugharimu sisi
Waislamu ni kuendekeza migogoro baina yetu na kufanya mambo yasiyo ya
kistaarabu katika Jamii,” alisema Sheikh Jongo.
Alisema baadhi ya kesi zilizopo mahakamani
zilizofunguliwa na Waislamu dhidi ya wenzao ni dalili ya kushuka kwa
maadili na hivyo kuwa kichocheo cha kudumaza maendeleo ya Waislamu.
Pia alitaja ugomvi unaotokea ndani ya misikiti kuwa ni miongoni mwa mambo yasiyokubalika katika jamii ya Kiislamu.
Mwinyi
Akizungumza kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es
Salaam, Rais huyo Mstaafu alisema ili kudumisha umoja wa muda mrefu wa
Watanzania, ni vyema watu wa dini zote wakashirikiana katika kila jambo
ili kuimarisha mshikamano. “Ni vizuri kwa Watanzania wa dini zote nchini
kuondoa tofauti zao na kujenga umoja na mshikamano ili kudumisha amani.
Tumeshuhudia matukio mbalimbali yanayohusishwa na masuala ya kidini
kama; uchomaji moto wa makanisa yalitotokea Visiwani Zanzibar na Bara,
umwagiaji wa tindikali kwa viongozi wa dini...”
Akizungumza kwa hisia, Mzee Mwinyi alisisitiza
umuhimu wa Watanzania kuwa wamoja licha ya kuwa kila mtu ana dini
yake... “Ninaomba Waislamu na watu wa dini nyingine kuwa pamoja, tuondoe
tofauti zetu kwani sisi Watanzania ni watu tuliozoeleka kwa kuwa na
amani, nisingependa kuona dini zetu zinasababisha uvunjifu wa amani.”
“Mwenyezi Mungu hatukatazi, kushirikiana pamoja
hivyo kwa hiyo tushirikiane, tupendane na tuimarishe umoja wetu ambao
ndiyo sifa kubwa tuliyokuwa nayo kwa muda mrefu.”
Lindi
Akihutubia katika Maulid yaliyofanyika kimkoa
kwenye Uwanja wa Ilulu Mjini Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Dk Nassor
Hamid alisema ni wajibu wa jamii kutambua kuwa amani na utulivu wa nchi
umetokana na umoja na mshikamano uliojengwa ambao hautakiwi kuchezewa na
mtu, kikundi, taasisi wala vyama vya siasa.
Dk Hamid aliwataka viongozi wa dini zote kutoa elimu ya maadili kwa waumini wao ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa jamii.
Alisema kuna mambo mbalimbali yameanza kujitokeza
katika jamii kama mavazi yasiyozingatia maadili ambayo si utamaduni wa
Kitanzania na kwamba mambo hayo yanachangia ushawishi wa ngono zembe na
kuongezeka kwa maambukizo ya Ukimwi.
“Ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda amani na
utulivu huo ili nchi yetu iendelee kutukuka kuwa ni kisiwa cha amani na
utulivu japo wapo baadhi ya watu wameanza kutaka kuharibu sifa hiyo.”
Songea
Sheikh wa Msikiti wa Wilaya ya Songea, Ruvuma,
Abdallah Kitete amesema kuna kila sababu ya waumini na wanasiasa
kuhubiri amani kwani pasipo vitu hivyo hakuna utawala...”Huwezi kutawala
watu sehemu ambayo haina amani....”
Aliitaka jamii ijitahidi kuiga mwenendo wa Mtume
Muhammad (SAW), alivyoishi na watu wa dini zote bila kuwabagua huku
akiwa mstari wa mbele kuhubiri upendo, amani na mshikamano na ndiyo
maana dini yake ilienea dunia nzima.
KWA HABARI ZAIDI====>BOFYA HAPA
KWA HABARI ZAIDI====>BOFYA HAPA